Dodoma.Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Philipo Mulugo, amesema Serikali haijafuta daraja sifuri
katika matokeo ya mitihani taifa ya shule za sekondari na kwamba
ilichokifanya ni
kuondoa mrundikano wa madaraja.
Mulugo aliyasema hayo jana bungeni, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM).
Magige alitaka kufahamu kama kushusha
madaraja ni suluhisho la kuwaokoa vijana waliofanya vibaya katika
mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.
Mapema katika swali lake la msingi,
Magige, alitaka kufahamu kama Serikali ina mkakati wa kuanzisha mpango
maalumu hasa wa ufundi kwa wanafunzi waliofanya vibaya katika mitihani
ya kidato cha nne mwaka jana.
Akijibu swali hilo, Mulugo alisema hawajashusha madaraja wala kuweka viwango tofauti na ilivyokuwa awali.
“Tumeongeza madaraja ili kuwatambua
watoto, kulikuwa na mrundikano katika daraja moja. Serikali haijafuta
division ziro na wala hakuna division V, ipo division I, II,III, IV na
ziro kama kawaida,” alisema.
Alisema uamuzi wa kushusha madaraja,
hauna lengo la kuwaokoa wanafunzi wanaofanya vibaya na badala yake,
unalenga katika kuondoa mrundikano wa alama katika daraja moja.
Alitoa mfano wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kuwa lilikuwa linapanga daraja F kuanzia alama 0 hadi 34.
Alisema kulikuwa hakuna ufuatiliaji wa
maendeleo ya mwanafunzi kama kanuni inavyosema kuwa lazima kuwe na
ufuatiliaji wa asilimia 50 kwa 50 .
Alisema kanuni hiyo inataka kutunzwa kwa
alama 50 katika ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi na katika
mtihani ya kumaliza shule asilimia 50.
Alisema wameanza kuyaweka madaraja kwa kutofautiana kwa alama 10 kila daraja.
Alisema bado daraja la ufaulu litaendelea kuwa 40 ama alama C.
ata hivyo, baada ya kumaliza kujibu
swali hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliiagiza Serikali kupeleka
bungeni kauli ya waziri kuhusiana na suala hilo.
“Naibu Waziri nenda mtuletee kauli ya Serikali kuhusiana na utaratibu huo ili kupata majibu yanayoridhisha,” alisema
Kuhusu wanafunzi waliofanya vibaya mwaka
jana katika mitihani yao, Mulugo alisema Serikali haitaanzisha mpango
maalumu wa ufundi kwa vijana hao.
Alisema badala yake, Serikali inawashauri wazazi kuwashawishi watoto kurudia mtihani wa kidato cha nne.
Kwa mujibu wa Mulugo, kwa mwaka huu, jumla ya watahiniwa 60,507 wa kujitegemea wamejisajili kufanya mtihani wa kidato hicho.
No comments:
Post a Comment